Rais Samia awasihi Watanzania kufuata misingi bora ya Hayati Rais Mwinyi

0
43

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ataendelea kuyaishi na kuyaenzi maono ya Rais Mstaafu, Hayati Ali Hassan Mwinyi kwa kusimamia ustawi wa wananchi, kushamirisha sekta binafsi, kutenda haki na kuwa na ustahimilivu.

Ameyasema hayo wakati akishiriki hafla ya mazishi ya Kitaifa ya Hayati Rais Mwinyi yaliyofanyika katika Uwanja wa Amani Abeid Karume ambapo amesema licha ya Hayati Mwinyi kuwa kiongozi katika vipindi vigumu kisiasa na kiuchumi, aliweza kuhakikisha utulivu na kufanya mageuzi makubwa katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.

“Kwa hulka yake ya ustahimilivu, Mzee Ali Mwinyi aliweza kuliongoza jahazi la Tanzania linaloheshimu haki za binadamu na utawala bora, na kuruhusu maoni tofauti na yale yaliyozoeleka ya Serikali,” ameeleza Rais Samia.

Rais Samia ameongeza kuwa Hayati Rais Mwinyi ana mchango endelevu uliozisaidia Serikali za awamu zilizofuatia, kwani ndiye aliyehamasisha uwekezaji kutoka sekta binafsi na soko huria zilizochangia katika ukusanyaji mapato.

Aidha, Rais Samia amewasihi Watanzania kuishi kwa kufuata misingi bora ya maisha na malezi na kuyachukulia maisha ya Hayati Rais Mwinyi kama funzo katika malezi ya vijana kwa kuzingatia maadili ya dini na hofu ya Mungu.

Send this to a friend