Rais Samia awasihi Yanga kumaliza mzozo na Fei Toto

0
40

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa viongozi wa klabu ya Yanga kumaliza mvutabo wa kimkataba unaoendelea kati yao na mchezaji wa klabu hiyo, Feisal Salum.

Ameyasema hayo katika hafla ya kuipongeza timu ya Yanga kama sehemu ya kutambua mchango na juhudi zao walizoonesha katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Sifurahii kusikia mnakuwa na mizozo na wachezaji, na sitaki kusema mengi nataka niwaambie kuwa hii issue ya Fei Toto embu kaimalizeni ili tuangalie mbele sasa, haipendezi klabu kubwa kama hii iliyofanya kazi nzuri inakuwa na kaugomvi na katoto,” amesema.

Aidha, Rais Samia amewaahidi waendeshaji wa mashindano ya Ndondo Cup kuangalia namna ya kuunga mkono mashindano hayo kwa kuwa huko ndiko vipaji vya wachezaji hutengenezwa.

Rais wa FIFA aipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu

“Nimekuwa nikifuatilia sana mashindano ya Ndondo Cup lakini pia Yamle Yamle kule Zanzibar, ni mashindano ambayo yanakuza vipaji kuja kulisha timu zetu kubwa za kitaifa.

“Nikitambua kuwa kule [Ndondo Cup] ndiko kunakozalisha vipaji katika mchezo huu wa mpira wa miguu, nataka niwaambie waendashaji wa mashindano haya kwamba niko pamoja nanyi na nitaangalia namna ya kuwashika mkono ili muendelee kusonga mbele,” ameongeza.

Katika juhudi za kuunga mkono michezo nchini, Rais Samia amesema Serikali imejipanga kujenga uwanja wa kisasa wa ndani (Indoor sports Arena) na kuufanyia ukarabarati mkubwa uwanja wa Benjamini Mkapa kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka barani Afrika na TFF.

Send this to a friend