Rais Samia awataka watumishi wa Sekta ya Ardhi kubadilika na kuachana na vitendo vya rushwa

0
6

Rais Suluhu Hassan amewataka watumishi wa Sekta ya Ardhi nchini kubadilika na kuachana na vitendo vya rushwa pamoja na maamuzi yasiyo ya haki yanayowasababisha wananchi kusumbuka na kunyimwa haki zao kwa maslahi binafsi ya baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Machi 17, 2025, wakati wa uzinduzi wa Sera ya Ardhi ya Mwaka 1995, toleo la mwaka 2023. Akiwahimiza watumishi wa sekta hiyo kuwa waadilifu na kukubali kubadilika ili kuhudumia nchi kwa uaminifu.

“Wenzetu mlioko kwenye sekta hii ya ardhi, niseme ukweli kwamba hamsemwi vizuri na jamii. Mnasemwa kwa kugawa kiwanja kimoja kwa watu zaidi ya mmoja, wakati mwingine kutokana na mazingira, lakini mara nyingine kwa makusudi. Rushwa inawafanya mfanye vitendo vya hovyo sana. Niwaombe kila mmoja aseme na moyo wake: ‘Naenda kubadilika na kuhudumia nchi yangu,” amesema Rais Samia.

Akiendelea kusisitiza umuhimu wa mabadiliko, Rais Samia amekemea vikali ucheleweshaji wa hati za umiliki wa ardhi kwa makusudi, vitendo vya rushwa miongoni mwa maafisa ardhi, pamoja na ukiukwaji wa sheria kwa maslahi binafsi, akieleza kuwa mfumo mpya wa E-Ardhi, ambao ameuanzisha, unapaswa kuwa suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi kutokana na utendaji mbovu wa baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu.

Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa ardhi ya Tanzania ni mali ya Watanzania pekee, huku wageni wakiruhusiwa kuitumia kwa madhumuni ya uwekezaji au shughuli nyingine, lakini kwa utaratibu wa ukodishaji, bila kuwa na miliki ya kudumu ya ardhi hiyo.

Pamoja na hayo, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Ardhi kwa kubadilika katika utendaji wake, kutoka kuwa wizara inayosifika kwa migogoro na uzembe wa makusudi, hadi sasa kuwa wizara inayochochea maendeleo ya wananchi.