Katika siku yake ya tatu ya ziara ya kikazi mkoani Kigoma, Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la Msingi la Upanuzi wa Bandari Ndogo ya Kibirizi mkoani Kigoma ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 69.5 na inahudumia mkoa wa Kigoma na nchi jirani.
Mradi huo ni sehemu ya mradi mkubwa unaohusisha Bandari za Tatu ambazo ni Kibirizi, Ujiji na Bandari Kuu ya Kigoma unaogharimu TZS bilioni 32 ikijumuisha ujenzi wa gati, majengo ya kupokea mizigo, jengo la abiria na ofisi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Rais Samia ameelekeza Wizara ya Ujenzi kuratibu ujenzi wa barabara ya kisasa ya kuingia kwenye bandari hiyo huku akielekeza ofisi ya mkuu wa mkoa kuondoa vibanda vilivyojengwa nje ya Bandari na kutoa mchoro wa ujenzi wa soko la kisasa.
Aidha, amesema Serikali imedhamiria kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwenye mkoa wa Kigoma kupitia miradi ya maendeleo ili uwe kitovu cha biashara.