
Rais Samia Suluhu Hassan amesema mataifa ya nje ambayo hayashiriki katika maono ya Tanzania yanapaswa angalau kuheshimu uhuru wa taifa, akisisitiza kuwa uamuzi wa Watanzania haupaswi kubezwa na mtu au taasisi yoyote ya nje.
Ameyasema hayo leo wakati wa sherehe za Mwaka Mpya wa Mabalozi pamoja na mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania, Wawakilishi wa Heshima na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa, katika hafla inayofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
“Wale ambao hawashiriki maono yetu, ninawaomba, angalau, waheshimu uhuru wa taifa letu. Sauti ya Watanzania imesikika kupitia sanduku la kura, na sauti hiyo lazima iheshimiwe,” amesema Rais Samia.
Aidha, ameeleza hatua za Serikali katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa, ikiwemo kuanzia wizara maalum ya vijana, kuwasamehe watuhumiwa 1,787 waliohusishwa na machafuko ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, kuunda Tume Huru ya Uchunguzi, na kuahidi kuanzisha Tume ya Maridhiano kama sehemu ya mchakato wa Katiba Mpya.
Rais Samia ameendelea kwa kusema kuwa, uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi, huku Pato la Taifa likikaribia asilimia 6 kwa mwaka 2025, mfumuko wa bei ukiwa katika kiwango cha asilimia 3.3, na deni la taifa likiwa himilivu, chini ya ukomo wa asilimia 55.
Mbali na hayo, amebainisha kuwa serikali imejizatiti kuendeleza mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kuimarisha demokrasia, utawala bora na ustawi wa wananchi. Amesema lengo kuu ni kujenga taifa lenye mshikamano, linaloheshimika kimataifa na lenye uwezo wa kusimamia mustakabali wake bila shinikizo la nje.







