Rais Samia azindua Tawi la 230 NMB, uzinduzi watikisa Kizimkazi Festival

0
54

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, jana Agosti 30, amezindua Tawi la Benki ya NMB Paje, Mkoa wa Kusini Unguja, hapa Zanzibar, uzinduzi unaoendelea kupanua mtandao wa matawi ya benki hiyo nchini na kufikia 230, yanayohudumia zaidi ya Wateja Milioni 6.

Uzinduzi huo ambao ni sehemu ya Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival 2023), ulioweka rekodi ya mahudhurio makubwa ya viongozi waandamizi wa Serikali na wastaafu, umekuja siku 58 tangu Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango alipozindua tawi la 229 la Benki ya NMB Buhigwe mkoani Kigoma.

Rekodi ya mahudhurio makubwa ya viongozi waandamizi wa Serikali imewekwa katika uzinduzi wa NMB Paje, ambako ukiondoa Rais Samia, wengine waliohudhuria ni pamoja Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Gavana Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.

Viongozi wengine ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mizengo Pinda, pamoja na Mawaziri wa Wizara mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Rais Samia aliwasili tawini NMB Paje majira ya saa 10:15 alasiri na ilimchukua dakika chache Bi Zaipuna kumpa maelezo mafupi ya tawi hilo na NMB kwa ujumla, ambako alimweleza kuwa tawi hilo linaenda kumaliza changamoto ya wakazi wa Paje kusafiri umbali wa kilomita 60 kufuata huduma zetu za kibenki kwenye Tawi la Mwanakwerekwe.

“Karibu kutuzindulia Tawi la NMB Paje, ambalo ni la nne hapa visiwazi Zanzibar, lakini likiwa ni la 230 kwa mtandao mzima wa matawi yetu nchini Tanzania.

“Tuna imani kwamba tawi hili linaenda kuwasaidia sana wakazi wa mahali hapa, ambao awali walikuwa wanasafiri umbali mrefu wa takribani kilomita 60 kwenda Mwanakwerekwe kufuata huduma zetu za kibenki katika tawi letu kule.

“Tawi hili litatoka huduma zote za kifedha ikiwamo kufungua akaunti, kufanya malipo, kuweka ama kutoa fedha, huduma za bima, mikopo, pamoja na kubadili fedha za kigeni.

“Pia, wafanyakazi wetu wa tawi hili watatumia jengo hili kutoa Elimu ya Fedha kwa wananchi hasa wavuvi, wakulima wa mwani na wazalishaji chumvi, elimu ambayo tayari imeshaanza kutolewa hapa kabla hata ya uzinduzi huu unaofanyika leo,” alisema Bi. Zaipuna kumueleza Rais Samia.

Baada ya maelezo hayo, Mheshimiwa Rais alikata utepe kuashiria ufunguzi wa tawi hilo, kabla ya kuingia ndani kukagua miundombinu na Mifumo ya utoaji huduma ndani ya jengo hilo.

Akiwa ndani ya tawi, Rais Samia alitembezwa katika Ofisi za Vitengo na Idara mbalimbali, zoezi lililofanyika kwa dakika 15, kabla ya kuondoka hapo na kuingia kwenye Viwanja vya Paje, vilivyopo mita 50 tu kutoka hapo, alikozungumza na wananchi wakati wa kuubariki Usiku wa Samia, ambao ni sehemu ya Kizimkazi Festival.

NMB Paje linakuwa ni tawi la 133 katika kipindi cha karibu miaka 26 ya benki hiyo ambayo ilikuwa na matawi 97 wakati ikianzishwa mwaka 1997. NMB Tawi la Paje linakuwa ni la tatu kufunguliwa na benki hiyo mwaka huu 2023, likitanguliwa na matawi ya Kwa Mrombo jijini Arusha (Mei 3) na Buhigwe Kigoma (Julai 4).

Send this to a friend