Rais Samia Suluhu Hassan amesema amesikitishwa na viongozi wasio waadilifu na wanaozembea makosa yanayofanyika katika miradi mbalimbali ya maendeleo na wakisubiri hadi mwenge wa uhuru upite na kufichua makosa hayo.
Akizungumza leo katika kilele cha Maadhimisho ya Mbio za Mwenge yaliyofanyika katika uwanja wa Kaitaba Bukoba Mjini mkoani Kagera amesema viongozi hawachukui hatua yeyote pindi miradi inapokuwa mibovu na pindi inapokuwa haiendani na thamani ya fedha iliyotumika.
”Hapa kuna swali kubwa la kujiuliza, wakati miradi hii inajengwa viongozi tupo tunaona lakini hakuna kinachozungumzwa wala kinachosemwa mpaka mwenge wa uhuru upite, kwahiyo huu siyo mtindo mzuri. Niwaombe sana na niwaagize wale wote walioko katika nafasi mbalimbali za mamlaka kusimamia fedha za wananchi. Hii ni kodi ya wananchi inayoshushwa kwa ajili ya maendeleo yao na ni vyema ikasimamiwa vizuri” amesema.
Aidha, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa Zanzibar (ZAECA) kujitathmini kwanza kabla hawajaenda kushughulikia vitendo vya rushwa katika taasisi nyingine ili kutambua mapema vitendo viovu vinavyofanyika ndani ya taasisi hizo.
Mbali na hayo, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 23 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais Samia amewaomba Watanzania kuendelea kumuenzi kwa kupinga vitendo vya rushwa, ufisadi, chuki na kuenzi umoja na ushirikiano kama ambavyo aliyasisitiza enzi za uhai wake.