Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania waendelee kuchukua tahadhari kama zinavyoelezwa na wataalumu kuhusu ugonjwa wa Corona.
Aidha, amewatoa hofu wananchi kuwa Serikali itaendelea kuchukua tahadhari zote zinazotakikana ikiwemo vifaa vinavyoletwa nchini kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo na kama itaamua kuruhusu ama kutoruhusu chanjo.
Rais Samia amesema hayo leo Mei 14, 2021 wakati akihutubia katika Baraza la Eid lililofanyika Kitaifa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa pamoja na kumcha Mwenyezi Mungu, Waislamu na Waumini na Madhehebu mengine ya Dini wanapaswa kuendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa, na kwa wafanyabiashara kulipa kodi kama inavyostahili ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali za kijamii ambazo ni pamoja na afya, maji na elimu.
Ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kusimamia malezi na maadili bora ya vijana na pia ametoa wito kwa Waumini wa Madhehebu yote ya Dini nchini kuendelea kuheshimana na kuvumiliana ambayo ni moja sifa kubwa za Tanzania.