Rais Samia: Baadhi walichukulia ukimya wangu kuwa udhaifu

0
40

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa katika kipindi cha miezi sita ya kuiongoza nchi katika nafasi hiyo, ameitumia kujifunza namna mawaziri, naibu, makatibu na naibu mataibu wao wanavyoendesha wizara husika, na kwamba wapo waliotumia ukimya wake wakati anajifunza kuwa ni udhaifu.

Samia amesema hayo akizungumza mara baaada ya kuwaapisha viongozi watano aliowateua jana, ambao ni mawaziri wanne Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dodoma.

“Katika kipindi hicho pia, hao hao niliowataja, mawaziri, manaibu, makatibu wakuu, manaibu, walinisoma mimi pia…. Kati yao walichukulia ukimya na utulivu wangu kama udhaifu na wakaanza kufanya yanayowapendeza,” amesema Rais Samia huku akiongeza kwamba “lakini wengine waliuchukulia ukimya na utulivu wangu kama ni njia ya kufanya kazi na kuonesha wanaweza kufanya kazi.”

Amesema kwa kipindi hicho alikuwa anajifunza na kwamba sasa ameona, na kusisitiza kwamba serikali itaendeshwa kwa matendo makali na sio maneno.

“Ninaposema matendo makali wala sio kupigana mikwaju wala mijeledi ni kwenda kwa wananchi kutoa huduma inayotakiwa,” ameongeza Rais na kusisitiza kwamba hatofokeana na watu kwa sababu wote ni watu wazima na kwamba kalamu yake ndiyo itafanya kazi zaidi.

Aidha, amewataka viongozi hao aliowateau kwenda kufanya kazi na kwamba wasidhani kwamba wao ni bora kuliko walioondolewa, na kwamba uzuri wao utaonekana kupitia kazi watakazofanya.

Send this to a friend