Rais Samia: Baadhi ya machinga Kariakoo tutawahamishia Jangwani

0
4

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inajipanga kujenga soko jingine kubwa kama la Kariakoo katika eneo la Jangwani, Dar es Salaam kupitia fedha za mradi wa uendelezaji jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Ameyasema hayo leo Januari 30, 2025 wakati akishiriki hafla ya chakula cha mchana na waokoaji wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika eneo la Kariakoo mwezi Novemba mwaka jana.

“Maoni yetu ni kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanangu wamachinga tutawahamisha tuwapeleke kwenye soko lile la Jangwani, na wakafanye biashara zao kwa nafasi na vizuri,” amesema.

Aidha, amesema tukio la kuporomoka kwa jengo la Kariakoo limetoa funzo kubwa kwa serikali kuhusu umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa na kuhakikisha serikali inakuwa na utayari wa kukabiliana na dharura wakati wowote, lakini pia imepata somo juu ya namna biashara inavyoongozwa katika soko hilo.

“Utanuzi wa majengo, uongezaji wa nafasi unafanywa kwa msingi ule ule uliokuwepo mwanzo na si kuanza tena kujenga. Tunarefusha juu tuna chimba chini lakini kwa msingi ule ule uliokuwepo mwanzo, hii ni hatari,” amesema.

Katika hotuba yake, Rais Samia amemwagiza Waziri wa Biashara na Uwekezaji, Sulemani Jafo kuliangalia kwa kina suala la wageni kufanya biashara inayofanywa na wenyeji hapa nchini kwakuwa ni vijana wa Kitanzania kufaidika na fursa hizo.

Send this to a friend