Rais Samia: Changamkieni fursa za kujenga hoteli za Watalii

0
24

Rais Samia Suluhu Hassan ameihimiza sekta binafsi kuchangamkia fursa ya kujenga hoteli nyingi zaidi kwa ajili ya watalii kutokana na ongezeko la watalii wengi wanaoingia nchini ili kuondoa changamoto ya upungufu wa malazi kwa wageni.

Ameyasema hayo akifungua mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo ameitaka Serikali kupunguza vikwazo vingi katika kutoa vibali vya ujenzi wa hoteli ili kazi hizo ziende kwa haraka pamoja na sekta inayohusika kwenye utalii kufanya marekebisho katika maeneo mbalimbali ili watalii waweze kurudi nchini.

“Wageni waliokuja mwaka jana asilimia 30 pekee wamerudi mwaka huu, inamanisha watu wanakuja wanasema Tanzania inatosha hatuendi tena pamoja na vivutio tulivyonavyo. Kwa hiyo angalieni kasoro ziko wapi tufanye marekebisho, ili wageni wawe wanarudi na walete wenzao,” amesema Rais Samia Suluhu.

Aidha, amewaagiza viongozi wa ngazi za Wilaya na Mikoa kuendeleza majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kama inavyofanyika katika ngazi ya Taifa ili kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji katika maeneo yao na kisha kuwasilisha taarifa za utendaji wa mabaraza hayo katika kila robo mwaka.

Mbali na hayo, ameziagiza wizara na taasisi za udhibiti kuharakisha utekelezaji wa maboresho katika maeneo mbalimbali kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini ili kupunguza gharama, na kubadilisha fikra mbalimbali na mitazamo kwa sekta binafsi.

“Sekta binafsi ndio itakayotutoa kiuchumi, Serikali hatufanyi biashara lakini Sekta binafsi inafanya biashara, wajibu wetu kama Serikali ni kutengeneza mazingira bora ambayo yataleta chachu katika ufanyaji biashara na uwekezaji ili uchumi wetu ukue zaidi,” amesema.

Send this to a friend