Rais Samia: Elimu inayotolewa iwezeshe wahitimu kujiajiri

0
37

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema elimu inayotolewa katika taasisi za elimu inapaswa kuwawezesha wahitimu wa vyuo kuwa na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa, na kuwa tayari kuchangia maendeleo ya taifa mara wanapohitimu masomo yao.

Ameyasema hayo katika mahafali ya 52 Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo pia ametunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa ya Heshima katika Humanitia na Sayansi Jamii ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutokana na mchango wake katika maendeleo ya jamii.

Rais Samia amesema tayari chuo hicho kimeanza mchakato wa kupitia mitaala yake ili iweze kujikita zaidi katika kutoa elimu ujuzi na kutoa wito kwa vyuo vingine kuiga mfano huo.
“Nichukue fursa hii kutoa rai kwa vyuo vingine vyote ambavyo havijafanya hivyo, kuiga mfano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa manufaa ya taifa letu,” amesema.

Aidha, ameahidi kuwa Serikali inafuatilia na itatoa mchango wake katika kuweka sera na mchakato ambayo inajumuisha kuendelea kuongeza bajeti ya elimu na kupanua wigo wa Tanzania katika kupata elimu stahiki katika ngazi mbalimbali.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amebainisha kuwa katika udahili wa mwaka huu kwenye chuo hicho, asilimia 53 ni wanawake huku ikielezwa kuwa jumla ya idadi ya wahitimu katika ngazi ya Shahada ya Udaktari na Uzamili ni 1002.

Send this to a friend