Rais Samia: Hakuna fedha za kitoa ruzuku kwa vyama vyote

0
41

 

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali haina fedha ya kutoa ruzuku kwa kila chama na kuvitaka vyama vya Siasa kuacha kutegemea Serikali katika kujiendesha.

Amezungumza hayo leo Machi 21 Ikulu jijini Dar es salaam wakati akipokea taarifa ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa ambapo amesema kuwa ruzuku itatolewa kwa wale wanaochapa kazi.

“Ruzuku ipo kwa wale ambao kweli wanafanya kazi wapo bungeni wanachapa kazi, wale unawapa ruzuku waende wakajipange kufanya zaidi,” amesisitiza.

Aidha, Rais Samia amesema kama kila chama cha Siasa kitapewa ruzuku,  vyama vingi vya siasa vitaundwa kila baada ya muda mfupi ilimradi vipatiwe ruzuku, hivyo Serikali haitaweza na kuviomba vyama hivyo kutafakari namna  ya kufanya.

“Unapounda chama cha siasa umejipimaje? Utakiendeshaje? Unategemea Serikali ikiendeshe chama chako cha siasa? Hapana ni chama chenu cha siasa mmejiunda,” amesema Samia

Hata hivyo Rais Samia amewaasa viongozi kujenga uadilifu kwenye mioyo yao na kuacha nidhamu ya uoga.

Send this to a friend