Rais Samia: Hatuwezi kuunga umeme shilingi 27,000 kwa wananchi wote

0
22

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwamba haiwezekani wananchi wote wakaungiwa umeme kwa gharama ya shilingi ya 27,000 kwani gharama za umeme haziko hivyo, na hiyo ni moja ya sababu ya watu kucheleweshewa umeme.

Rais amesema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akipokea taarifa ya awali utekelezaji wa matumizi ya fedha za UVIKO-19, ambazo zilielekezwa kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa 15,000, miradi ya maji na afya.

Amesema uamuzi wa kutangaza kwamba kila mwananchi ataungiwa umeme kwa kiasi hicho cha fedha uliofanywa kipindi cha nyuma hauwezekani kwani unasababisha TANESCO kukosa fedha za kujiendesha.

“Kuna maeneo tutafanya hivyo kuwainua wananchi wetu, kuna maeneo lazima gharama ya umeme irudi pale pale,” amesema Rais.

Amemuagiza Waziri wa Nishati, January Makamba kutekeleza hilo, huku akieleza kwamba kwa muda mrefu waziri huyo aliogopa kulisema hilo.

“Kuna maeneo lazima gharama ya umeme ibebe uhalisia. Unampangia leo TANESCO aende akaunge umeme kwa kila mtu kwa shilingi 27,000, yeye anatoa wapi hizo fedha? Lazima aunge umeme kwa gharama inayopaswa kila mahali,” amesisitiza.

Hata hivyo amesisitiza kwamba kwenye maeneo ya vijijini gharama ibaki iliyopo sasa, na maeneo ya mijini iwe katika kiwango ambacho mwananchi ataweza kumudu.

Pamoja na hayo amesema kwa dunia ya sasa umeme kwa mwananachi sio anasa na ndio maana serikali kupitia TANESCO imeendelea kujiimarisha kwa kusambaza umeme vijijini.

Send this to a friend