Rais Samia: Jaji hakutenda haki sakata la wafugaji Lindi

0
29

Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza watendaji wa mahakama nchini kuziangalia kwa ukaribu mahakama za ngazi za chini ili wananchi waweze kupata haki wanazostahili.

Ameyasema hayo leo Mei 23, 2023 wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali wakiwemo majaji pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Maadili, Jaji Rose Aggrey Teemba Ikulu jijini Dodoma, ambapo amemuagiza kusimamia na kuongeza kasi zaidi katika kujenga maadili ya viongozi na watendaji hasa wa serikali.

“Sina wasiwasi kwenye ngazi za juu kabisa huko, jicho lako Jaji Mkuu liko karibu kabisa. Ngazi za chini, wale watendaji wa mahakama tunahitaji macho makali kabisa, bado mambo huko yanaendelea hovyo hovyo,” amesema Rais Samia.

Ameongeza, “tumesikia ile kesi ya Lindi kwamba wafugaji wamefanya makosa ya wazi wazi wamekamatwa kwenye makosa, Jaji akasema nakwenda huko huko kutizama na kurudi akasema hawana makosa, sasa utajiuliza kuna nini hapo.”

Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Watanzania wana hamu ya kuona kuwa wanatendewa haki katika mahitaji yao mbalimbali, hivyo Serikali imefungua progamu ya kuwasaidia Watanzania kujua haki zao inayojulikana kama ‘Samia Law Support Program’ ambayo imekusanya wadau wengi waliobobea kwenye masuala ya sheria ili kuwasaidia Watanzania wanaohitaji haki.

Send this to a friend