Rais Samia: JWTZ halikujengwa kwa misingi ya kuwa jeshi la uvamizi

0
19

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) halikujengwa katika misingi ya kuwa jeshi la uvamizi isipokuwa jeshi la wananchi, hivyo litaendelea kulinda amani na kuhimiza majirani kuhimiza amani katika nchi zao.

Akizungumza wakati akishiriki kilele cha Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam amesema jeshi hilo halijavamia nchi yoyote na halina mpango wa kufanya hivyo.

“Pamoja na amani iliyopo nchini, jeshi letu linaendelea kujiimarisha katika nyanja zote kuendana na misingi ya kuundwa kwake, dhamira yetu ni kujenga jeshi imara lililo tayari kwa hali zote wakati wowote,” ameeleza.

Aidha, amesema JWTZ limeshiriki na kufanikisha harakati za kuleta ukombozi barani Afrika ikiwemo kuyafundisha majeshi ya vyama vya ukombozi lakini pia kuwa mstari wa mbele kwenye uwanja wa vita vya ukombozi katika nchi za Msumbiji, Angola, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini ambapo leo hii nchi hizo ni uhuru.

“Baada ya ukombozi jeshi letu limeendelea kushiriki kikamilifu na kwa mafanikio makubwa kwenye operesheni mbalimbali za kulinda amani katika nchi mbalimbali ikiwemo Liberia, Sudan Darfur, Lebanon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Visiwa vya Comoro, Msumbiji na DRC,” amesema.

Katika hotuba hiyo, amewashukuru makamanda na wapiganaji wa JWTZ kwa moyo wa kizalendo na ushujaa huku akiongeza kuwa wananchi wanathamini mchango wao katika kuisaidia nchi.

Send this to a friend