Rais Samia: Kifo cha Membe kimeacha pengo kitaifa na kimataifa

0
24

Ris Samia Suluhu Hassan amesema kifo cha Bernard Membe kimeacha pengo kubwa si kwa taifa pekee bali hata katika mataifa aliyowahi kuyafanyia kazi.

Ameyasema hayo leo Mei 14, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akishiriki ibada ya kuaga mwili wa Membe, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, ambapo alifikwa na mauti Mei 12, mwaka huu kwa tatizo la upumuaji.

“Ndugu Membe alikuwa mtu muungwana sana, mchapakazi na aliyependa maendeleo ya nchi na wananchi wake, si tu kwa taifa lake, bali hata mataifa mengine,” amesema.

Rais Samia amewapa pole wafiwa wote na taifa kwa ujumla akimuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na kuiahidi familia ya hayati Membe kuwa Serikali iko pamoja nao katika kipindi chote cha msiba huo.

Aidha, viongozi mbalimbali waliotoa salamu zao akiwemo kiongozi wa Chama cha ACT-WAZALENDO, Zitto Kabwe amesema Membe alikuwa mstari wa mbele kutetea Watanzania wote bila kujali itikadi zao za vyama vya siasa.

“Tunakuaga leo, lakini ulikuwa mtu mwenye msimamo sana. Hukuogopa kusema lile uliloliamini, wakati mgumu sana wa maisha yako kisiasa ulikuwa ndio wakati mgumu sana wa kisiasa hapa nchi, ulisimama na watetezi wa demokrasia na watetezi wa haki za binadamu bila kupepesa macho,” amesema

Ameongeza, “mpaka umauti unakufika, haukuacha kulionesha taifa na dunia namna tunapaswa kuhusiana hata kama tunapingana kimawazo na mirengo ya kisiasa.”

Send this to a friend