Rais Samia Suluhu Hassan amewaomba Watanzania kutumia fursa zinazoletwa nchini kuitangaza na kuisemea vizuri Tanzania pamoja na kutumia fursa hizo kibiashira.
Ameyasema hayo leo Ikulu jijini Dar es salaam alipokuwa akipokea Kombe la Dunia la mashindano ya mpira wa miguu litakaloshindaniwa nchini Qatar.
“Kombe la Dunia kutembezwa Tanzania kuna maana kubwa kwa nchi yetu. Mchango wake kiuchumi na kijamii una umuhimu mkubwa na wa kipekee kwa fursa zinazoweza kupatikana, lakini kubwa kuitangaza nchi yetu,”amesema.
Aidha, amewaalika wageni wote waliofika nchini na kombe hilo, kutenga siku kwa ajili ya kufanya utalii uliopo Tanzania na kuwahidi kuwa hawatojutia kwa kufanya hivyo.
“Ni matarajio yangu kuwa wageni wote walioandamana na kombe hili, watafurahia kuwepo Tanzania kwa muda wa siku hizi mbili, lakini kwa wale wenye muda zaidi tunaomba mbaki mfanye utalii Tanzania, hamtajutia,” amesisitiza.
Ametumia nafasi hiyo kuipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa juhudi na ubunifu walioufanya kutumia Daraja la Tanzanite kuonesha mchezo wa fainali ya UEFA kati ya Liverpool na Real Madrid, huku akibainisha kuwa, tukio hilo limeonesha jinsi Tanzania ilivyo na vivutio vinavyoweza kutumika.
Kombe la Dunia linapitishwa katika nchi tisa barani Afrika, tano kati y hizo zimefuzu kushiriki mashindano hayo na nne, ikiwemo Tanzania, hazijafuzu.