Rais Samia kuajiri walimu wapya 7,000

0
15

Ili kuendana na kasi ya ujenzi wa madarasa mapya 15,000 yaliyojengwa nchini kote, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema serikali inakusudia kuajiri walimu wapya wapatao 7,000.

Rais ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza kwa simu na uongozi wa Shule ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam palipokuwa panafanya hafla ya kusherehekea kiongozi huyo kutimiza umri wa miaka 62.

Ameeleza kwamba anatambua sekta ya elimu ina mahitaji mengine, na kwamba serikali imekusudia kwenda hatua kwa hatua hadi kumaliza zote.

“Baada ya kujenga madarasa na kuyawekea ‘furnitures’ [samani], kinachofuata ni kuongeza ajira za walimu. Nitaongeza walimu 6,000 au 7,000 hivi, tutawaongeza na kuwasambaza ili waendane na ujengaji wa madarasa,” ameahidi Rais Samia.

Aidha, katika hatua nyingine ameahidi kwamba akienda Dar es Salaam atatembelea shule hiyo baada ya kuombwa na mmoja wa wanafunzi mwenye mahitaji maalum ambaye alitaka kuonana na Rais, Ikulu.

Ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wote waliomtakia heri katika siku yake ya kuzaliwa. Akizungumza mapema leo na TBC, Rais alisema kwamba wito wake muhimu kwa Watanzania ni kufanya kazi kwa bidii kwani nchi haijengwi na mtu mmoja, bali kila mmoja kwenye nafasi yake.

Send this to a friend