Rais Samia kufanya ziara ya kitaifa nchini Uturuki

0
38

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kitaifa ya siku tano nchini Uturuki kati ya Aprili 17 hadi 21, mwaka huu kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdoğan.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa AfrikaMashariki, January Makamba (Mb.) amesema mwaliko huo unafuatia baada ya miaka 14 kupita tangu Rais wa Tanzania kutembelea nchini humo na ni miaka saba tangu Rais wa nchi hiyo kutembelea nchini mwaka 2017.

Makamba amesema Tanzania na Uturuki zimekuwa na mahusiano mazuri ya kidemokrasia na kibiashara hivyo ziara hiyo itaimarisha zaidi mahusiano kwani Tanzania inahitaji mitaji, teknolojia na wawekezaji.

Wafanyabiashara wengi wa Tanzania wamekuwa wakienda kununua bidhaa Uturuki na sisi tumekuwa tukiuza bidhaa nyingi huko, hivyo la kwanza ni kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, kibiashara na kisiasa kati ya nchi hizo mbili,” amesema.

Aidha, amesema mbali na Rais Samia kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, pia atakwenda mjini Istanbul katika kongamano kubwa la kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki ambalo litakutanisha wafanyabiashara wa pande zote, ambapo Rais Samia atakutana na kampuni 15 nchini humo kwa ajili ya kuwashawishi kuchangamkia fursa zilizopo nchini.

“Kuna maeneo ambayo tunashirikiana nao yalitarajiwa kuwa maeneo zaidi ya 10 lakini hadi sasa tuna maeneo kama sita ambayo yamethibitishwa kuwa tutasainiana mikataba na hati za makubaliano, “ ameeleza Waziri Makamba.

Send this to a friend