Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeimarisha vituo vya utafiti na mashamba ya uzalishaji mbegu ili kufikia mwaka 2025 robo tatu ya mbegu za kisasa zitakazotumiwa na wakulima wa Tanzania zizalishwe nchini.
Ameyasema hayo wakati akijibu swali na mmoja wa vijana walioshiriki katika mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) lililouliza kuwa Serikali inajipangaje ili kuwavuta vijana kujiingiza katika sekta ya kilimo, mkutano uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Rais Samia amesema ili mkulima aweze kufanya vizuri na serikali iweze kutoa huduma za ugani zinazoeleweka, kila mkulima atapimiwa afya ya udongo katika vipindi tofauti ili kuwa na uhalisia wa aina gani ya mbegu na mbolea anazopaswa kutumia.
Ameongeza kuwa Tanzania imejizatiti katika kutengeneza bandari za Tanzania na kujenga barabara zinazounganisha wilaya, mikoa na nchi jirani ili mazao ya wakulima yaweze kufika kwenye masoko kwa wakati.
Majaliwa amuagiza Naibu Waziri Mkuu kushughulikia upatikanaji wa mafuta
Aidha, Rais Samia amekiri kuwa bado kuna changamoto ya upatikanaji wa masoko zinazochangiwa na kutofahamu mahitaji halisi ya soko la ndani na nje ya nchi pamoja na muunganiko wa soko, hivyo Serikali imeanza kuweka jitihada kwa baadhi ya mazao kama korosho ambayo imeleta matokeo chanya.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Tanzania imekusudia kulisha dunia, hivyo imejiwekea mipango thabiti ya kuwezesha vijana na wanawake kupata mikopo itakayowawezesha kutimiza vyema shughuli zao za kilimo.