Rais Samia Suluhu Hassan leo amefanya ziara ya kushtukiza kwa kutembelea soko la Kariakoo mkoani Dar es Salaam.
Amewatembelea wafanyabiashara wanaouza bidhaa zao hasa vyakula ndani ya soko kuu na kujionea msongamano mkubwa wa bidhaa, wafanyabiashara na wananchi wanaokwenda kununua bidhaa.
Wafanyabiashara hao wamelalamikia tatizo la ugumu wa uingizaji wa bidhaa kutokana na njia za kuingia sokoni kufungwa na wafanyabiashara wengine ambao wamepanga bidhaa zao njiani, tozo kubwa za vizimba, ushuru wa bidhaa zinazoingia sokoni na gharama za usafishaji wa bidhaa kutokana masoko mengine.
Baada ya kujionea hali halisi, Rais Samia ameelezea kusikitishwa kwake na hali hiyo na amesema Serikali itafanya tathmini ya uendeshaji wa soko hilo ili kurekebisha dosari zilizopo ikiwemo kuratibu uingizaji wa mizigo, mpangilio wa bidhaa sokoni na kuboresha usafi.
Ameagiza kusimamishwa mara moja kwa uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo ili kupisha uchunguzi kufuatia malalamiko mbalimbali yaliyotolewa na wafanyabiashara dhidi ya viongozi hao, lakini wakati hatua hizo zinachukuliwa amewataka wafanyabiashara kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na sheria.