Rais Samia kuongoza mjadala wa kitaifa wa Nishati safi ya kupikia

0
16

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuongoza kongamano la mjadala wa kitaifa wa Nishati safi ya kupikia itakayofanyika Novemba 01 na 02, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Waziri wa Nishati, January Makamba wakati akitambulisha kongamano hilo leo Oktoba 12, 2022 amesema mjadala huo utaleta suluhu kwa Watanzania na namna sahihi ya upikaji pamoja na upatikanaji wa mifumo ya kisera, kisheria, kikodi na kiutawala ili kuondokana na matumizi yasiyo salama ya nishati.

Dhima ya kongamano hilo ni;

1. Kutafakari na kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu hali halisi ya nishati ya kupikia nchini.
2. Kupata uzoefu na elimu kutoka katika nchi nyingine zinazoendelea zilizofanikiwa katika suala hili.

3. Kuchambua na kutathmini hatua za kisera, kisheria, kifedha na kiudhibiti zitakazosaidia kufanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

4. Kupata muafaka baina ya wadau wote kuhusu hatua mbalimbali na wajibu wa kila mmoja, katika safari ya kuelekea kwenye nishati safi ya kupikia.

5. Kutengeneza jukwaa la kujenga mashirikiano baina ya wadau wa nishati safi ya kupikia.

Ili kushiriki mkutano huu, washiriki wanapaswa kujisajili kupitia tovuti maalumu ya www.cleancookingconference.co.tz na kupata taarifa nyingine zinazohusiana na mkutano huo.