Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kutengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Ameyasema hayo wakati wa kufunga mafunzo ya siku sita ya uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Julius Nyerere Kibaha mkoani Pwani.
Rais Samia amesema kitendo cha viongozi wawili wa serikali, Hanafi Msabaha (DC) na Tatu Said Issike (DED), kushindwa kutekeleza majukumu yao kiliwalazimu wakazi wa Mtwara kuukana uanachama wa Chama cha Mapinduzi na kurejesha kadi zao za uanachama.
“Leo nitatengua uteuzi wa mkuu wa wilaya ya Mtwara, siwezi kuvumilia kadi za chama zirudishwe, na bado DC na DED wapo karibu, ukiwauliza kwanini kadi nyingi za chama zinarudishwa wanakwambia kuna wapinzani wengi. Kwa hiyo nini? Watu hao ni Watanzania; hawahitaji chochote?” amehoji.