Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.) amesema Seneti ya Chuo Kikuu cha Ankara ambacho ni chuo kikuu cha pili kwa ukubwa nchini Uturuki, kimeamua kwa kauli moja kumtunuku Rais Samia Suluhu Hassan Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Uchumi.
Amesema uamuzi huo ni kutambua uongozi wa kipekee wa Rais Samia katika kuendeleza mageuzi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ambayo yameboresha ustawi wa Watanzania, kukuza sifa ya Tanzania duniani kote na kuendeleza uhusiano wa kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo Uturuki.
“Hafla ya kutunuku tuzo hiyo itafanyika kesho tarehe 18 Aprili 2024, mchana, katika Chuo Kikuu cha Ankara na itaongozwa na uongozi mzima wa chuo hicho na kuhudhuriwa na mawaziri, wanadiplomasia, kitivo na wanafunzi,” ameeleza.
Ameongeza kuwa baada ya hafla hiyo, Rais Samia atapokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais Recep Tayyip Erdoğan kwa ajili ya mazungumzo rasmi, kabla ya kuelekea Istanbul kwa ajili ya Kongamano la Biashara na viongozi wa wafanyabiashara wa Uturuki, ambalo pia litahudhuriwa na Makamu wa Rais wa Uturuki na mawaziri mbalimbali.
Shahada hiyo itakuwa ya nne kwa Rais Samia kutunukiwa baada ya awali kutunukiwa nyingine na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).