Rais Samia kuunda Tume kushughulikia suala la Ngorongoro
Rais Samia Suluhu amesema ataunda Tume mbili ambapo moja itachunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala ya ardhi yaliyolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro, na nyingine itaangalia utekelezaji wa zoezi zima la uhamiaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi la Ngorongoro.
Ameyasema hayo wakati alipokutana na kuzungumza na Viongozi wa Kimila wa Jamii ya Masai (Malaigwanani) kutoka Tarafa ya Ngorongoro na maeneo jirani, kwenye kikao kilichofanyika Ikulu ndogo ya Arusha ambacho kimefanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao kufuatia kuwepo kwa malalamiko dhidi ya baadhi ya maamuzi ya Serikali yanayohusu eneo la Ngorongoro.
Aidha, Rais Samia ameiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la Ngorongoro.
Mbali na hayo, Rais Samia amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na jamii hiyo.