Rais Samia: Lazima tufanye kazi ili tusitegemee mataifa ya nje

0
12

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi aliyekuwa na fikra na falsafa za dhana ya kujitegemea wakati wa uongozi wake.

Rais Samia amesema hayo leo wakati akihutubia katika Mdahalo wa Kitaifa wa kuadhimisha Miaka 100 ya Kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere.

Aidha, Rais Samia amesema Mwalimu Nyerere aliamini Tanzania na Mataifa mengine ya Afrika hayawezi kuwa na nguvu ya kuijiamulia mambo yake endapo yataendelea kuwa na uchumi tegemezi hivyo hatuna budi kuwajibika kwa kuchapa kazi na kutumia vizuri rasilimali tulizonazo ili tujitegemee kiuchumi.

Amesema ili kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi, Serikali ya Awamu ya Sita inafanya jitihada mbalimbali kama kuimarisha huduma za afya, miundombinu ya elimu na viwango vya elimu.

Aidha, Rais Samia amemuelezea Mwalimu Nyerere kama kiongozi aliyejenga misingi imara ya amani, umoja, na mshikamano tuliyonayo hivi sasa ambayo inaendelezwa na kila awamu ya uongozi.

Rais Samia ametoa wito kwa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kuwa kitovu cha uandishi na uhifadhi wa historia ya harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika na maeneo yaliyohusishwa katika harakati za ukombozi yatambuliwe na kuendelezwa ili yatumike kama kivutio cha utalii wa kihistoria.

Katika maadhimisho hayo, Rais Samia alizindua vitabu vitatu ambavyo ni: Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: Chemchemi ya Fira za Kimapinduzi; Misingi ya Falsafa, Itikadi na Sera za Chama Cha Mapinduzi na Development as Rebellion chenye Juzuu Tatu za The Making of a Philosopher Ruler, Becoming Nationalist na Rebellion without Rebels.

Send this to a friend