Akizungumzia chanjo ya UVIKO-19 katika Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema lengo la Serikali yake ni kuhakikisha wananchi wote wanachanjwa ili kupata kinga ya ugonjwa huo.
Aidha, ameziomba nchi za SADC kushawishi kampuni zinazozalisha chanjo kuridhia vibali na teknolojia zao zitumike ili kuruhusu chanjo kuzalishwa katika nchi mbalimbali ili kukidhi mahitaji yaliyopo.
Rais Samia amesema ni lazima kushirikiana katika kubadilishana mbinu na uzoefu na kuwaelimisha wananchi kuhusu dhana potofu dhidi ya chanjo hizo pamoja na kuwahimiza kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na janga hilo.
Pia ameziomba Nchi zilizoendelea na Taasisi za Kifedha za Kimataifa kuendelea kutoa misamaha au kurefusha muda wa ulipaji wa madeni kwa Nchi zinazoendelea mpaka pale janga hilo litakapokwisha.
Kuhusu masuala ya uongozi amewasihi viongozi wa SADC kushirikiana katika kuendeleza jitihada za kuwainua na kuwawezesha wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi na maamuzi katika nchi zao.
Aidha, Rais amewafahamisha viongozi wa SADC kuwa katika mkutano wa Generation equality uliofanyika hivi karibuni nchini Ufaransa ulimchagua kuwa kinara (champion) wa Masuala ya Haki za Kiuchumi za Wanawake (Women Economic Rights and Justice), hivyo kuomba ushirikiano kutoka kwao ili yeye na timu yake iweze kutekeleza jukumu hilo kikamilifu.