Rais Samia: Mabalozi fanyeni kazi kwa matokeo, msisubiri matukio

0
49

Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza mabalozi kufanya kazi kwa kujituma katika vituo vyao vya kazi walivyopangiwa pasipo kusubiri matukio maalum ili kulinufaisha Taifa.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaapisha mabalozi wateule iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, Rais Samia amesema mambo yanayofanyika ubalozini hubeba taswira ya taifa, hivyo matendo yanayofanywa na mabalozi yanaweza kufaidisha au kulifedhehesha taifa.

“Katika nchi nyingine Mabalozi wetu sijui niseme hawajui wanachokifanya, wapo tu, nilishakutana na Rais mwenzangu ndani ya Nchi za Afrika, ndani ya SADC akaniambia nibadilishie balozi uliyeniletea hata kazini haendi, mikutano hashiriki yupo yupo tu hatuelewi, Tanzania hatujawazoea hivyo sasa labda ubadilishe nikamwambia nimekusikia,” ameeleza.

ACT yataka Dkt. Slaa na wenzake wapelekwe mahakamani au waachiwe huru

Aidha, ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumetokea mahitaji mapya ndani ya dunia kama vile; mabadiliko ya tabia ya nchi, mapinduzi ya nne ya viwanda, matumizi ya akili bandia, uchumi wa buluu, utalii endelevu, mahitaji ya diaspora, masuala ya haki za binadamu n.k, hivyo ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje kuainisha majukumu, wajibu na stahili za kila balozi ili kulinda maslahi ya taifa katika maeneo hayo iwe kwa fursa au kukabiliana na changamoto zake.

Mbali na hayo, Rais Samia amewaasa mabalozi wateule kupita katika sekta mbalimbali hapa nchini kabla ya kwenda katika vituo vyao vipya vya kazi ili kujua mikakati na mipango mbalimbali inayotekelezwa katika sekta hizo pamoja na kubeba taarifa zitakazowasaidia katika vituo wanavyokwenda.

Send this to a friend