Rais Samia: Mafanikio yaliyopo nchini ni matokeo ya ushirikiano wa Kitaifa

0
3

Rais Samia Suluhu Hassan amesema mafanikio yaliyopatikana nchini katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita yanatokana na utekelezwaji wa matakwa ya maendeleo na ustawi ya wananchi wa Tanzania kama yalivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.

Rais Samia ameyasema hayo mara baada ya kupokea Tuzo Maalum ya Heshima aliyotunukiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni ishara ya kutambua uongozi wake mahiri uliolenga kuleta maendeleo jumuishi na ustawi wa Taifa.

Akielezea shukrani zake kufuatia kupokea Tuzo hiyo, Rais Samia amesema kwake tuzo hiyo ni ishara ya kuthamini kazi ya pamoja kati ya mihimili ya dola, viongozi wa Serikali na wananchi wote kwa ujumla waliotoa ushirikiano wa karibu katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Sita na kuwezesha nchi kupata maendeleo.

Aidha, amelipongeza Bunge la Tanzania kwa dhamira yake ya dhati ya kuisimamia Serikali kupitia mijadala ya bajeti, kwa kupitisha sheria muhimu, pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali ambao umeongeza tija katika utendaji kazi katika ngazi zote.

Naye, Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amesema Tuzo hiyo imetolewa kwa niaba ya wabunge wote nchini kama ishara ya kutambua uongozi wake.

Hali kadhalika, ameeleza kuwa kupitia uongozi wa Rais Samia, Taifa limeshuhudia mageuzi makubwa katika kuimarisha Muungano, utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, sambamba na maendeleo makubwa kwenye sekta za elimu, afya, madini, utalii, uchukuzi, kilimo, nishati na diplomasia ya kimataifa.