Rais Samia: Mafunzo kwa watumishi yanaongeza ufanisi kwenye kazi
Rais Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wizara ya Utumishi na wizara inayoshughulika na kazi na ajira kuzungumza na waajiri kwa upande wa sekta binafsi ili kuwaruhusu Makatibu Mahsusi pamoja na Watunza Kumbukumbu na kujiunga na mafunzo ili kutanua wigo wa taaluma zao.
Ameyasema hayo leo kwenye kilele cha mkutano wa kitaaluma wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) pamoja na Menejimenti ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) uliofanyika katika viwanja vya Fumba, Zanzibar.
“Kujiunga na mafunzo ya aina hii kwanza mnapata kutanua wigo wa taaluma yenu lakini pili mnapata kufunzwa yale ambayo wengi wenu hamkuwa mnayajua,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa makatibu mahsusi pamoja na watunza kumbukumbu kuiga mfano wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kuanzisha mfumo utakaowasaidia wakati wa shida ambao utalindwa kisheria na kutumika kwa matumizi watakayo kubaliana.
Mbali na hayo, ametoa wito kwa watumishi wote wa Serikali na sekta binafsi kuweka kipaumbele suala la nidhamu na uadilifu kazini ili kuwa na ufanisi zaidi wa kazi.
“Ufanisi maana yake ni kuikamilisha kazi vile inavyotakiwa, kwa kiwango kinachotakiwa na wakati unaotakiwa. Ukiwa na nidhamu na uadilifu utazalisha kazi kwa wakati kwa kiwango kinachotakiwa na muda unaotakiwa,” ameeleza.