Rais Samia: Magari ya TASAF yasiende kubeba magunia ya mikaa

0
12

Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka halmashauri na Wakurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo (TASAF) kusimamia magari 241 yaliyotolewa kwa mamlaka za maeneo ya utekelezaji kwa shughuli za TASAF.

Akizungumza hayo leo Juni 1, jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kukabidhi magari hayo, Rais Samia amesema utunzaji wa magari hayo ni jukumu la halmashauri, na kueleza kwamba yatafungwa mfumo wa ufuatiliaji ili kujua sehemu yalipo, yanachofanya pamoja na usalama wake.

“Magari haya yasiende kubeba magunia ya mikaa na kuni, lakini mbaya zaidi magari haya yanakwenda kubeba abiria. Madereva wanaokabidhiwa tumeshayaona huko kwenye maeneo nyakati za jioni yanatoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, wanaita wenyewe ‘somba somba’ anayemkuta njiani ingia nauli ngapi,lipa kama unavyolipa nauli ya gari,” amesema Rais Samia.

Aidha, baada ya magari hayo mapya kugawiwa, Rais ameagiza magari yote yaliyotolewa taarifa kuwa ni mabovu yarudishwe yakiwa na vifaa vyote muhimu katika ofisi za TASAF tawi la Dar es Salaam.

Hata hivyo, ameisisitiza TASAF kutoa msaada wa elimu kwa jamii ili kuwatoa watu kwenye umaskini wa fikra na kuwasaidia kuishi maisha yasiyo duni.

Send this to a friend