Rais Samia: Mama Mkapa aligundua uwezo wangu wa siasa

0
24

Rai Samia Suluhu Hassan amemshukuru mke wa Hayati Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa kwa kuwainua wanawake zaidi ya 6,000 wanaofanya biashara ndani na nje ya Tanzania, pamoja na kumsaidia kugundua uwezo wake katika siasa.

Ameyasema hayo leo wakati akishiriki katika sherehe ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa taasisi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (Silver Jubilee of Equal Opportunities for All Trust Fund – EOTF ) katika ukumbi wa JNICC Dar es Salaam na kueleza kuwa, nguvu ya kuingia kwenye siasa ni baada ya maneno na ushauri wa Mama Mkapa.

“Nikiwa ndani ya gari la Mama Mkapa [mwaka 1999] aliniambia Samia [Suluhu] nimekuona toka umekuja [kwenye taasisi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote 1999], nimekuona unavyokwenda na unavyofanya, wewe ni mwanasiasa mzuri sana, uchaguzi unaokuja ungejaribu kuingia,” amesema.

Aidha, amesema amefarijika kuona mwamko wa wanawake na vijana wa kujituma katika kujiendeleza kiuchumi, kijamii na kuisaidia EOTF kutekeleza matakwa yake tangu kuanzishwa kwa taasisi.

Amebainisha kuwa, matokeo ya wanawake kujiunga na EOTF imesaidia kuondokana na umasikini kwa kuanzisha vikundi vya wanawake ili kujipatia kipato, na pia kushughulika na masuala ya afya.

Mbali na hayo Rais Samia amewasihi Watanzania kuonesha ukarimu kwa watalii wanaokuja kufanya utalii nchini, ili wanaporudi nchini kwao, waweze kuwashawishi wengine kutembelea Tanzania.

“Niwaombe sana ndugu zangu, tupokee wageni wetu [watalii] vyema ili waondoke na kumbukumbu zitakazokwenda kuwashawishi wengine waweze kuja katika nyakati mbalimbali.”

Send this to a friend