Rais Samia: Mawaziri jueni mipaka ya mamlaka yenu

0
56

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kufanya kazi kwa kuzingatia misingi iiyowekwa ikiwemo kuheshimu katiba, kujua mipaka na kutunza siri za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameyasema hayo leo Oktoba 03, 2022 katika hafla ya kuwaapisha mawaziri wateule iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kujua ukomo wa mamlaka walizopewa, hivyo wanapotaka kuvuka mipaka yao ni lazima kupata ruhusa kutoka kwenye mamlaka ya juu.

Rais Samia afanya mabadiliko Baraza la Mawaziri

Aidha, Rais Samia amesema viongozi hao wanapaswa kutumikia kwa usawa pande zote mbili za muungano kama ilivyo katika viapo vyao, na kwamba wanapaswa kutunza siri za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kujua jinsi ya kuzitumia siri hizo katika utendaji wao wa kazi.

“Linaloamuliwa na Serikali, wewe kama waziri ni lako na unatakiwa ulibebe ukalifanyie kazi kwa misingi ile uliyoelekezwa. Huwezi kusema nimeelekezwa hivi mimi sikutaka hivi, lakini imebidi nifanye hivi kwa sababu nimeelekezwa, huwezi kujitoa,” amesema Rais Samia.

Viongozi walioapishwa leo ni aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Angellah Kairuki kuwa Waziri wa TAMISEMI pamoja na Dkt. Stergomena Tax kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Send this to a friend