Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kupungua kwa kina cha maji katika maeneo mbalimbali nchini kunachangiwa na sababu kuu mbili ambazo ni ukaidi wa binadamu na kudra za Mwenyenzi Mungu.
Akizungumza katika Maadhimisho wa Jubilei ya Miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza amesema kuwa licha ya viongozi kutumia nguvu nyingi kuelimisha na kudhibiti shughuli za kibindamu kwenye vyanzo vya maji, bado kuna watu wameendelea kukaidi.
“Ninatambua miji yetu mikubwa inakabiliwa na uhaba wa maji unaopelekea upungufu wa maji na mgao wa umeme. Hali hii imetokana na mambo makubwa mawili, ubishi wa binadamu na kudra za Mwenyenzi Mungu,” amesema Rais Samia.
Akizungumzia mkoa wa Dar es Salaam amesema kwamba maji katika Mto Ruvu Chini yamepungua kwa nusu ya kiwango kinachotakiwa, na hivyo kupelekea huduma hiyo kwa wakazi wa mkoa huo kupungua pia.
Akielezea mipango ya kurejesha huduma hizo katika hali ya kawaida amesema operesheni imefanyika na kubaini wapo watu wanaochepusha maji kutoka kwenye mito kwenda kwenye maeneo yao kwa ajili ya kilimo, jambo ambalo linaweza kutafsiriwa kuwa ni uhujumu wa makusudia wa kuzuia maji kwenda kuchakatwa ili kuwafikia wananchi.
Amesema kwamba mgao huo wa maji utapungua kutokana na hatua zilizoanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wanaofanya shughuli zao kwenye vyanzo hivyo pamoja na kupunguza mchanga.
Mbali na kilimo amesema kwamba wananchi wamekuwa na tabia isiyokubalika ya kuingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji, ambapo kama ng’ombe mmoja anatumia lita 40 kwa siku, maelfu ya ng’ombe watatumia maji mengi zaidi.
“Mkitusikia tunatoa watu, wafugaji kwenye mabonde msitulaumu, lengo ni hili, kuhifadhi ikolojia ya maeneo yale, lakini pia kupata maji ya kutosha kupeleka kwa wananchi,” amefafanua Rais Samia akiongeza kuwa ukataji uchomaji miti pia ni sababu inayosababisha ukame.
Ameagiza viongozi kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaofanya shughuli kwenye vyanzo vya maji pamoja na kuweka ulinzi kwenye vyanzo hivyo.