Rais Samia Suluhu Hassan ametajwa na jarida la Time la nchini Marekani miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi zaidi kwa mwaka 2022.
Katika orodha hiyo iliyojumuisha kuanzia wasanii, wafanyabiashara, wabunifu hadi wanasiasa, Rais Samia ameelezewa na Rais Mstaafu wa Liberia na mshindi wa tuzo ya Nobel, Ellen Sirleaf, kuwa kiongozi aliyechochea mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika mwaka mmoja alioiongoza Tanzania.
Sirleaf ameeleza kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia, mlango wa majadiliano umefunguliwa kwa wapinzani wa kisiasa, hatua zimechukuliwa kurejesha imani katika mfumo wa kidemokrasia, jitihada zimefanyika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na waliokatisha masomo wamerejeshwa na wanawake wana mtu wa kumtazama.
Aidha, amemuelezea Samia kuwa Septemba 2021, miezi michache baada ya kushika ushukani alitoa hotuba ya kipekee katika jukwaa la Umoja wa Mataifa.
“Kama Rais wa kwanza mwanamke kwenye historia ya nchi yangu,” alisema, “mzigo wa matarajio ya kuufikia usawa wa kijinsia unayaelemea mabega yangu.”
Sirleaf amehitimisha simulizi yake akieleza kuwa, baada ya kusikia maneno hayo hakuweza kujizuia kutafakari namna mabega ya viongozi wanawake yalivyo imara na mabadiliko ambayo yanaweza kuleta.
Mbali na Rais Samia, watu wengine kwenye orodha hiyo ni pamoja na mwigizaji Channing Tatum, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, Rais wa China Xi Jiping na Rais wa Marekani, Joe Biden.