Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imepanga kurudisha nyongeza za mishahara za kila mwaka kwa wafanyakazi utaratibu ambao ulikuwa umesimama kwa muda mrefu.
Amesema hayo katika kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi, Mei Mosi ambayo kitaifa yamefanyikia mkoani Morogoro, ambapo ameahidi kuendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kazi serikalini na katika sekta binafsi.
“Kuna nyongeza za mishahara za mwaka ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimesitishwa, nikaona mwaka huu tuzirudishe. Kwa hiyo wafanyakazi wote mwaka huu [..] kuna nyongeza za mishahara za kila mwaka, na tunaanza mwaka huu na tutakwenda kila mwaka kama ilivyokuwa hapo zamani,” amesema Rais Samia Suluhu.
Serikali yatoa bilioni 230 za ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi
Aidha, amesema katika kurekebisha sheria za kazi na kanuni, Serikali imeandaa sera ya taifa ya usalama na afya mahali pa kazi, pia imeanzisha chombo mahsusi cha Serikali cha kusimamia masuala ya usalama na afya kazini, pamoja na kuanzisha mfuko wa fidia kwa wafanyakazi, ikiwa ni kuendana na masharti na mikataba ya kazi.
Mbali na hayo, Rais Samia amemwagiza Waziri Mkuu na Waziri wa Elimu kusimamia ufufuaji wa vituo vya E- Education ili walimu wapate elimu ya matumizi ya vishkwambi na kutumia ipasavyo kufundishia.
Naye Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Hery Mkunda amemshukuru Rais Samia kwa mambo makubwa aliyoyafanya kwa wafanyakazi, huku akiomba punguzo au ondoleo la kodi katika maeneo wanayokatwa hasa hasa kwenye upande wa marupurupu ya nauli za likizo, ‘overtime’ na maeneo mengine.