Rais Samia: Mradi wa huduma za mawasiliano vijijini utasaidia kukuza pato la taifa

0
40

Rais Samia Suluhu amesema kukamilika kwa mradi wa kufikisha huduma za mawasiliano ya simu vijijini kutasaidia kukuza pato la taifa kutokana na kuongezeka kwa wigo wa matumizi ya teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA) pamoja na mawasiliano katika sekta nyingine.

Ameyasema hayo Mei 13, 2023 jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini ambapo Serikali na watoa huduma za mawasiliano zimetia saini mikataba ya kufikia huduma za mawasiliano katika vijiji 3,704 vyenye wakazi milioni 15.

Rais Samia amesema kupitia mradi huo utasaidia kukuza biashara vijijini, kukuza elimu, ulinzi na usalama pamoja na kubadilisha teknolojia vijijini ambapo wakulima na wafanyabiashara watatoka kwenye matumizi ya simu za tochi na kuingia kwenye matumizi ya simu janja ili kuwawezesha kupata taarifa mbalimbali duniani.

Msigwa: Rais Samia amechangia pakubwa kukamilika kwa Ikulu Chamwino

“Tunachokifanya leo kinakwenda kukuza sekta mbalimbali za nchi yetu, tunakwenda kukuza maendeleo mijini lakini na kule vijijini, ili twende kwa kasi katika maendeleo,” amesema.

Aidha, Rais Samia amesema pamoja na changamoto za kifedha wanazopitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupeleka umeme kwenye vitongoji, amewaagiza kuhakikisha umeme unakuwepo katika minara yote ili kuwezesha kushuka kwa gharama za bando.

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema katika mradi huo, minara 758 inakwenda kujengwa katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara ambapo vijiji 1407 katika wilaya 127 zitapata huduma za mawasiliano ambapo hadi kukamilika kwa mradi huo utachukua muda wa miezi 18.

Send this to a friend