Rais Samia: Ni wakati wa Afrika kusimulia hadithi zetu wenyewe

0
30

Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi za Afrika kuandika upya simulizi kuhusu bara la Afrika kwa kusimulia hadithi zao wenyewe kutoka kwa mitazamo yao na kuonesha taswira chanya na halisi ya bara hilo.

Katika hotuba yake katika Mkutano wa Kimataifa wa 23 wa Baraza la Utalii Duniani (WTTC) uliofanyika jijiji Kigali, Rais Samia amesema serikali za Afrika lazima zichukue hatua kufanya maendeleo makubwa katika sekta ya utalii, ikiwa ni pamoja na masuala ya masoko na uendelezaji wa chapa, utafiti, na uhifadhi.

“Afrika inapaswa kusimulia hadithi zake yenyewe kwa maneno yake na kuweka simulizi chanya kuhusu bara letu. Hatuwezi kuendelea kukaa katika zama hizi za habari za uongo, tunapaswa kusimama na kuweka rekodi sawa,” amesema.

Amesisitiza kuwa Afrika lazima ichukue fursa za utalii wa mazingira (ecotourism) na kuwekeza katika maeneo yaliyolengwa ili kufikia hadhira ya kimataifa.

Aidha, amesema Afrika inapaswa kuweka kipaumbele na kusaidia juhudi za kuhifadhi maeneo ya kitamaduni, vitu vya sanaa na mila zake kwa ajili ya vizazi vijavyo, ikiwa bara hilo bado linataka kuendelea kutegemea vivutio vyake vya asili.

Katika hotuba hiyo, amesema utalii unachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi nyingi za Afrika akitolea mfano Tanzania, sekta ya utalii inachangia hadi asilimia 17.2 ya pato la taifa (GDP) na asilimia 25 ya mauzo yote ya nje.

“Huu ni mchango mkubwa kutoka chanzo kimoja, na inaonyesha kuwa Afrika inaweza kutumia utalii kukuza uchumi na kutoa fursa za ajira,” ameeleza.

Send this to a friend