Rais Samia: Nitahakikisha Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia

0
48

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ataendelea kuwawezesha Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ili ifikapo mwaka 2030 zaidi ya asilimia 88 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Ameyasema hayo leo alipozungumza kwa njia ya simu na wanawake waliojitokeza katika kongamano la kumpongeza kwa kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia, mazingira na afya ya mama na mtoto yaliyofanyika katika Ukimbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.

“Ahadi yangu kwenu ni kuhakikisha asilimia kubwa ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia na hili nitalivalia njuga, kuhusu masuala ya jinsi na watu wenye makundi maalum nitaendelea kusimamia kuhakikisha tunaondokana na changamoto zilizopo,” amesema.

Naye, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kumuunga mkono Rais Samia ili aweze kutimiza maono yake ya kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, utunzaji wa mazingira pamoja na uimarishaji wa afya ya mama na mtoto kwa tija na ufanisi mkubwa.

Aidha, amewataka watendaji wote wanaosimamia miradi ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira wahakikishe wananchi wote wanashirikishwa kikamilifu katika kampeni zote ili nchi ipate matokeo ya haraka.

Katika mkutano huo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliendesha harambee ambayo ilifanikisha kupatikana kwa shilingi milioni 120 kwa ajili ya kumwezesha Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Send this to a friend