Rais Samia: Ripoti za CAG zinaimarisha utendaji serikalini

0
35

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka zinachangia kuimarisha na kuboresha utendaji ndani ya Serikali na mashirika ya umma.

Amesema hayo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma wakati akipokea ripoti ya CAG pamoja na Taarifa ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka 2022/23 ambapo ameeleza kuzifanyia kazi ipasavyo dosari mbalimbali zilizotolewa katika maeneo yaliyoibuliwa.

Katika ripoti iliyosomwa na CAG, Charles Kichere, moja kati ya mambo yaliyoibuliwa ni pamoja na Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) kupata hasara ya TZS bilioni 56.64, sawa na ongezeko la asilimia 61 kutoka hasara ya TZS bilioni 35.24 iliyoripotiwa katika mwaka wa fedha 2021/22.

Kwa upande wa deni la Serikali amesema kufikia Juni 30, 2023 lilikuwa shilingi trilioni 82.25, sawa na ongezeko la asilimia 15 kutoka shilingi trilioni 71.31 kwa mwaka 2021/2022. Deni hilo linajumuisha deni la ndani la shilingi trilioni 28.92 na deni la nje la shilingi trilioni 53.32.

Aidha, CAG ameeleza kuwa ofisi yake imebaini kuwa hasara katika Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imepungua kwa asilimia 94 na kufikia shilingi milioni 894 mwaka 2022/23 kutoka shilingi bilioni 19.23 mwaka uliopita, huku Shirika la Reli Tanzania (TRC) likipunguza hasara kwa asilimia 47.32, kutoka hasara ya TZS bilioni 190.01 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 100.7 mwaka 2022/23.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP. Salum Hamduni amesema Tanzania ni moja kati ya nchi 28 duniani zinazoonesha kuimarika katika mapambano dhidi ya rushwa katika kipindi cha mwaka mmoja, pia ni miongoni mwa nchi sita kati ya nchi 180 zinazoonesha kuimarika katika kupungua kwa vitendo vya rushwa.

Send this to a friend