Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuchochea ukuaji wa sekta ya uvuvi kupitia mipango na programu mbalimbali ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.
Amesema miongoni mwa mipango hiyo ni utekelezaji wa mradi wa kielelezo ikiwemo ununuzi wa meli ya kisasa za uvuvi katika bahari kuu, ujenzi wa bandari za uvuvi katika maeneo ya Kilwa Masoko mkoani Lindi na Bagamoyo.
Hayo yamebainishwa leo katika uzinduzi wa ugawaji wa vizimba vya kufugia samaki na boti za kisasa kwa ajili ya wavuvi wa Kanda ya Ziwa, jijini Mwanza ambapo Boti 55 za uvuvi wa kisasa zinatarajiwa kukabidhiwa kwa wanufaika 989 pamoja na vizimba 222 vinavyotarajiwa kugaiwa kwa wanufaika 1,213 katika mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Geita.
“Bandari hizo zitakapokamilika zitakuwa miongoni mwa bandari kubwa na za kisasa za uvuvi katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwahiyo tunajipanga hivyo, Kilwa tayari tumeanza na Bagamoyo hatuna muda tutaanza,” amesema Rais Samia.
Aidha, ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na sekretarieti za mikoa na halmashauri kudhibiti na kutokomeza vitendo vya uvuvi haramu pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria wavuvi wanaokiuka taratibu za uvuvi salama.
Vile vile, amesema kundi la vijana na wanawake linaongoza kushiriki kwenye ajira zisizo rasmi hivyo serikali inarasimisha shughuli zao kwa kuwawezesha kupata zana na nyenzo za kisasa ili kujikimu kiuchumi.