Rais Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na mvua zinazoendelea kuleta athari katika baadhi ya maeneo hapa nchini Serikali inakwenda kufanya uchunguzi wa kina ili kujua sababu za maafa hayo.
Kauli hiyo ameitoa katika ibada ya kumbukizi ya miaka 40 tangu kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika nyumbani kwake Monduli mkoani Arusha leo.
“Licha ya kuwa baadhi ya maeneo yaliyoathirika ni yale ambayo yamekuwa yakikumbwa na mafuriko ya kujirudia kwa nyakati tofauti, kwakuwa kiasili ni maeneo yenye mabonde au njia za asili za maji, bado naona kuna sehemu kama serikali tunaweza kuboresha. Ni ukweli kuwa hatuwezi kuzuia mvua kubwa na mafuriko moja kwa moja lakini tunaweza kupunguza madhara kuimarisha jitihada za kukabiliana na athari za mvua na mafuriko,” amesema.
Ameongeza kuwa “baada ya mvua hizi na hali ya kawaida kurejea, Serikali tutafanya uchunguzi wa kina kubaini sababu halisi za mafuriko kwenye maeneo hayo na tuweze kuchukua hatua zitakazoondoa tatizo hilo kwa muda mrefu.”
Rais Samia amewataka Watanzania kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua pamoja na kuendelea kutoa misaada kwa waathirika wa mafuriko na pia kuwa watulivu na kushirikiana na viongozi katika maeneo yao.
Aidha, amewataka viongozi na Watanzania kwa ujumla kufuata mienendo bora ya Hayati Edward Sokoine kwani katika kipindi cha uhai wake alisisitiza uwajibika na kujituma serikalini kwa ajili ya maendeleo ya nchi.