Rais Samia: Serikali yangu si ya maneno ni vitendo

0
40

Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali ya Awamu ya Sita inataka kuona vijana wa Kitanzania wakijenga uchumi imara pamoja na kujenga ustawi wa maisha yao na familia zao.

Ameyasema hayo leo Juni 24, 2023 jijini Arusha wakati alipowasili na kusalimiana na wananchi wa mkoa huo ikiwa ni katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya yatakayofanyika kitaifa mkoani humo Juni 25, mwaka huu.

“Tunataka kuona vijana wa Kitanzania wakiwa wako ‘busy’ kuzalisha mali na kujenga ustawi wa maisha yao na kujijengea uchumi wenye hadhi, uchumi imara kwa wenyewe na familia zao,” amesema Rais Samia Suluhu.

Aidha, amesema Serikali inafanya jitihada mbalimbali ikiwemo kufungua nchi na kukaribisha sekta binafsi ili zije zifanye kazi na Tanzania katika maeneo mbalimbali ili kuzalisha ajira kwa vijana na kujenga kesho yao iliyo njema.

Mbali na hayo, Rais Samia amesema Serikali yake haina maneno mengi bali inafanya kazi kwa vitendo na kuangalia wapi inakusudia kwenda ili kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Send this to a friend