Rais Samia: Sina kundi katika kufanya uteuzi wa viongozi

0
45

Rais Samia Suluhu Hassana amesema hana kundi lolote katika kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali isipokuwa anachotaka ni kuona walioteuliwa wanafanya kazi na kuisogeza nchi mbele.

Ameyasema hayo leo baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali kwenye hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Mwanzo nilipoanza kuwaapisha wakuu wa mikoa niliwaambia mnatarajia ningewachagua kwa makundi, lakini mimi kama Samia sina kundi na mkijitazama humo haya makundi mnayoyajua makundi yenu nyote mmo humo ndani. Ninachotaka Watanzania kwa pamoja tufanye kazi tuisogeze nchi yetu,” amesema.

Aidha, amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kushughulikia matatizo yanayowahusu wananchi na si kusubiri viongozi wa juu kufika katika maeneo yao na kufanya hivyo kwa kuwa inajenga picha mbaya kwa wananchi kwa kujiona kuwa hawasikilizwi.

“Nataka niwakumbushe kwamba nyinyi ndio marais wa maeneo yale, shida yoyote ya eneo lile ni shida yako. Kama nilivyo mimi nina mawaziri nina makatibu wakuu, na nyinyi kule mnao, mna wakuu wa wilaya, mna ma-RAS, ma-DAS, hao wote wamewekwa wakusaidieni kazi,” ameeleza.

Katika hotuba hiyo, Rais Samia amesema hivi sasa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeanza kufanya tathmini juu ya utendaji kazi wa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri ili kujua nani hafanyi vizuri.

Send this to a friend