Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imechangia askari 1,489 katika misheni 16 za ulinzi wa amani duniani na kwamba iko tayari kutoa mchango zaidi.
Ameyasema hayo wakati akishiriki sherehe za mwaka mpya 2023 kwa mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo amesema Tanzania itaendelea na dhamira yake ya kushiriki katika ulinzi wa amani kwa kuchanguia vikosi pamoja na misaada mingine.
Aidha, Rais Samia amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua ambapo kwa mwaka 2022 pato la taifa limekua kwa asilimia 4.7 ukilinganisha na asilimia 4.3 mwaka 2021, huku mwaka 2023 mategemeo ya ukuaji wa pato la taifa ukitegemewa kuwa na ukuaji wa zaidi ya asilimia 5.
Kwa upande wa miradi, amebainisha kuwa kutoka mwezi Julai mpaka Novemba 2022 kumekuwa na ongezeko la miradi ambayo imefikia 132 yenye thamani ya dola bilioni 3.16 ambayo ni ongezeko la asilimia 22.2 ikilinganishwa na idadi ya miradi iliyosajiliwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2021.