Rais Samia: Tanzania tuna udhaifu katika uendeshaji wa mashtaka

0
25

Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Tume ya Haki Jinai kushughulikia udhaifu uliopo katika ukamataji wa watuhumiwa, upelelezi, uendeshaji wa mashtaka pamoja na mambo mengine yanayofanyika magerezani ili kutoa haki kwa wananchi.

Ameyasema hayo leo wakati akipokea taarifa ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai hapa Tanzania kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Othman kwenye hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Huu ndio udhaifu wetu kwanza, tukubali kuwa Tanzania tuna udhaifu huo na hatuna budi kuufanyia kazi ili haki iweze kutendeka,” amesema.

Pamoja na hayo, amesema kuna udhaifu wa ubobezi kwenye mfumo wa upelelezi katika pande zote mbili za muungano na kuielekeza tume kushirikiana kwa pamoja na kufanyia kazi madhaifu yaliyopo na kuziimarisha taasisi, kuzipa weledi ili kutoa haki inayostahili.

Rais Samia: Nchi za jirani zinatamani fursa tuliyoipata

Aidha, katika hotuba hiyo ameelekeza tume kulitazama Jeshi la Polisi katika nyanja mbalimbali ikiwemo mishahara, stahiki zao, vikokotoo na kadhalika ili kuwawezesha kufanya kazi zao vizuri.

“Jeshi la Polisi liko kule chini kwenye community [jamii] sasa hivi wana Polisi Jamii ambayo iko kule chini, na wale watu wanafanya kazi vizuri, na wengine wanafanya kazi vibaya,” ameeleza.

Naye, Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande ambaye ni mwenyekiti wa tume hiyo ya haki jinai ametoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo kufanyiwa marekebisho ya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 ili kuweka tafsiri ya kifungo cha maisha kwa kuonesha muda maalum wa kifungo na kuweka ukomo wa adhabu ya kifungo hicho ili kutoa matumaini mapya kwa watuhumiwa.

Send this to a friend