Rais Samia: Tukio la kuanguka kwa ghorofa Kariakoo limetupa funzo

0
33

Rais Samia Suluhu Hassan amesema hadi kufikia asubuhi ya leo, idadi ya vifo vilivyosababishwa na jengo kuporomoka katika eneo la Kariakoo imefikia 20, ambapo Serikali imeshirikiana na familia kuwastiri marehemu huku waliojeruhiwa wakibakia watatu pekee hospitalini.

Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo hilo kujionea taratibu za uokoaji zinazoendelea, amesema tukio hilo ni moja ya matukio ya kutisha yaliyowahi kutokea Tanzania, na kuwapongeza Watanzania kwa kujitoa kwao kusaidia katika zoezi la uokozi.

Aidha, amesema tukio hilo limetoa ujumbe mkubwa kwa Serikali na jamii nzima katika kuangalia hali ya usalama wa majengo ya Karikoo, ambapo tayari amemwelekeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuunda tume itakayofanya ukaguzi wa majengo hayo.

“Niseme kwamba, tukio hili limetupa ujumbe mkubwa wa kuangalia usalama wa majengo yetu katika eneo la Kariakoo. Wakati naoneshwa, ukiliangalia jengo lenyewe lilivyojengwa kuta zake na nondo, jengo halikusimamiwa vizuri,” amesema Rais.

Ameongeza kuwa, “Niwaombe watu wote tunaohusika kwenye mambo haya; Serikali kuu, halmashauri, viongozi wa Serikali za mitaa, Asasi za kiraia na wananchi wote kwa ujumla, tuseme kwa pamoja kwamba matukio ya namna hii yasijirudie kwa sababu tukio hili ni huzuni kubwa sana kwa taifa letu,” amesema.

Rais Samia amewaambia wafanyabiashara walioko mbali na eneo lililopata maafa kuendelea na biashara, huku wale walio katika eneo la hatari lifungwe ili wataalam wa uokoaji waendelee na zoezi la kufumua jengo hilo.

Send this to a friend