Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyabiashara kutumia Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kukuza biashara zao pamoja na kuzitumia taasisi za Serikali kufanikisha azma ya kufanya biashara kwenye nchi za nje na hasa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).
Akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo, Rais Samia amesema wafanyabiashara kutoka Tanzania wanapaswa kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nje ili waweze kukuza biashara zao.
“Tangu yaanze mwaka 1963, maonesho haya ya Sabasaba yamejizoelea sifa nyingi barani Afrika na duniani kwa ujumla. Nafurahi kwamba maonesho ya mwaka huu yamekutanisha zaidi ya kampuni 3,486 kama yalivyochambuliwa hapa ya ndani na nje ya nchi,” amesema.
Ameongeza kuwa “matunda ya kuimarika kwa ushirikiano tumeshaanza kuyaona, mwaka 2023 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC kimesajili miradi 504 mwaka jana yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 5.68. Hii ni kwa sababu watu wanakuja Tanzania wanaona fursa wanashiriki maonesho na kuvutika kuja kuwekeza.”
Aidha, amesema Serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara wanazokumbana nazo nchini pamoja na kutoa fursa kwa wafanyabiashara wote wenye maoni ya kuboresha na kuisaidia nchi kuyafikisha katika wizara husika ya viwanda na biashara ili maoni hayo yaweze kufanyiwa kazi.
Pia, ametoa rai kwa Watanzania kutembelea na kushiriki katika maonesho hayo makubwa na kutumia vizuri programu mbalimbali zinazoandaliwa na Serikali katika kupata wadau wa biashara na wawekezaji.