Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Indonesia zimekubaliana kuimarisha urafiki na ushirikiano uliopo katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya watu wa pande hizo mbili.
Akizungumza katika mapokezi ya Rais wa Indonesia, Joko Widodo, Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo pia wameshuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano baina ya nchi hizo, amesema licha ya uwepo wa uhusiano mkubwa wa kidiplomasia, kuna mengi zaidi yanaweza kufanyika ili kutumia fursa zilizopo na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano hasa upande wa uchumi.
“Tumekubaliana kukuza biashara na uwekezaji kwa kuzileta pamoja sekta za umma na binafsi na hapa tumedhamiria kuimarisha zaidi ushirikiano wetu katika viwanda, kilimo, nishati, madini, mafuta na gesi, uvuvi, utalii na sekta za ukarimu na kubadilishana maarifa na teknolojia,” amesema.
Ameongeza kuwa “Kama mnavyojua Indonesia ni kati ya nchi zenye mashirika bora ya kibiashara yanayomilikiwa na Serikali, na kama mnavyojua ni dhamira yangu pia kwamba mashirika yetu haya lazima tuyajenge yawe mashirika madhubuti ya kibiashara.
Rais Samia atoa maelekezo kufanikisha mageuzi mashirika ya umma
Aidha, amesema katika mazungumzo yao amekaribisha uamuzi wa Indonesia wa kufufua Kituo cha Mafunzo kwa Wakulima Vijijini (Farmers’ Agriculture and Rural Training Centre (FARTC), kilichopo Mikindo mkoani Morogoro ambacho kimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuelimisha wakulima na kutoa mafunzo kwa wataalam wa kilimo.
Mbali na hayo, amemwomba Rais Widodo kushirikiana katika kukuza uchumi wa buluu ambao umepewa kipaumbele na Serikali ya Zanzibar na hasa katika ujenzi wa badari kubwa ambayo itatoa huduma mbalimbali unaohusu uchumi wa buluu.